Afrika Haiwezi Kuendelea Kutegemea Dawa Kutoka Nje ya Bara Asema Rais.

0

Rais William Ruto amesema kuwa Kenya inachukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuna upatikanaji wa bidhaa za dawa.

Rais amesema kuwa hatua hizo zinajumuisha kuwezesha almashauri ya taifa ya udhibiti kuafikia kiwango cha tatu cha shirika la afya duniani WHO ili kuhakikisha dawa hizo zinaafikia ubora, usalama na ufanisi.

“Serikali inachukua hatua mahsusi kuimarisha mfumo wa dawa nchini kwa kuongeza uwezo wa mamlaka ya udhibiti ili kuhakikisha bidhaa zinazotengenezwa Kenya zinaaminika kimataifa kwa ubora na usalama wake.” Rais alisema.

Aidha amesema kuwa Afrika haiwezi kuendelea tena kutegemea dawa kutoka nje ya bara la Afrika akisema kuwa Afrika hukabiliwa na asilimia 25 ya magonjwa ila hutengeneza chini ya asilimia 6 ya dawa.

Kadhalika ameangazia umuhimu wa Afrika kuwa na mifumo imara ya kujitegemea katika kukabiliana na dharura za kiafya huku akisema hatua hiyo itasaidia kuunda nafasi zaidi za ajira, kukuza viwanda vya ndani na kuimarisha uchumi wa mataifa ya Afrika.

Wakati uo huo, Rais amesema kuwa Bara la Afrika lina uwezo mkubwa wa kutoa suluhu kwa changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu wa sasa ikiwa litapewa nafasi sawa katika maamuzi ya kimataifa.

Aidha, amekosoa hatua ya kuendelea kuliondoa Bara la Afrika katika uwakilishi wa kudumu ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema hali hiyo ni kosa kubwa linalodhoofisha ushirikiano wa kimataifa na haki ya usawa kwa mataifa yote duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here