Huduma za matibabu Jijini Mombasa zinatarajiwa kutatizika kufikia saa sita usiku tarehe 4 Machi 2026, kufuatia kutamatika kwa notisi ya siku saba iliyotolewa na madaktari mnamo siku ya Jumanne tarehe 24 Februari 2026 kabla ya kuanza kwa mgomo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari Nchini (KMPDU) Davji Atella, madaktari wako tayari kuanza mgomo huo mara tu muda wa notisi utakapokamilika usiku wa manane.
“Tuko tayari kuanza mgomo ambao tulitoa notisi yake wiki iliyopita na ambayo inaisha tarehe tatu Machi usiku wa manane.” Atella amesema,
“Tumegundua kuwa madaktari wako tayari kwa asilimia mia moja kuanza mgomo. Tunataka kukutana na serikali ya kaunti ili kujadili masuala yote tuliyowasilisha. Haya ni mambo ambayo hatuwezi kuyajadili upya,” ameongeza Atella.
Kulingana na KMPDU, mgomo huo umechochewa na masuala mawili makuu, ikiwemo madai kwamba serikali ya kaunti ya Mombasa imeingiza siasa katika sekta ya afya.
Muungano huo pia umelalamikia kuondolewa ofisini kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Coast General, Daktari Iqbal Khandwalla wiki iliyopita kwa madai ya utepetevu.
Serikali ya kaunti ilimsimamisha kazi Daktari Khandwalla kufuatia kifo cha mgonjwa mwenye umri wa makamo aliyejulikana kwa jina Ali Kibwana katika hospitali hiyo.
Ali Kibwana alikuwa mfanyakazi katika ofisi ya Mbunge wa Mvita Mohammed Machele, ambaye aliongoza maandamano ya wakazi kushinikiza kuondolewa kwa Khandwalla.
Iwapo pande husika hazitafikia mwafaka kabla ya usiku wa manane, wakazi wa Mombasa huenda wakakumbwa na changamoto kubwa ya kupata huduma za matibabu katika hospitali za umma.









