Wakenya kwenye mitandao ya kijamii sasa wamemtaka Rais William Ruto kutohusisha taifa katika vita vinavyoendelea katika nchi za Ghuba zikiwemo Iran, Israel, Qatar, Falme za Kiarabu, Bahrain, Kuwait, Saudi Arabia, Jordan na Iraq kufuatia kuongezeka kwa mvutano baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Katika machapisho yao, baadhi ya wananchi wamesema Kenya haina uwezo wa kijeshi wa kuingia katika vita vya kisasa vinavyohusisha makombora ya masafa marefu na mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga.
“Mheshimiwa Rais, unaingilia vita ya mataifa makubwa yanayotumia makombora ya kisasa ilhali sisi tuna silaha ndogo tu… nyamaza mkuu.”
“Omba Iran isiskie haya, juu inaweza kuichukulia kwa uzito.” Woywoy Kamama Domnic amesema kwenye mtandao wa Facebook.
Wengine wameeleza wasiwasi wao wakidai kuwa Rais anaepuka kutaja moja kwa moja mataifa yanayohusika na mashambulizi hayo.
“Rais anaonekana kuogopa kuchukua msimamo thabiti, analaani hali ya Mashariki ya Kati bila kutaja mhusika. Je, analinda maslahi fulani maalum?” alisema Purity Mwende
“Mheshimiwa Rais, mashambulizi hayajitokezi yenyewe unaogopa kuitaja Marekani na Israel?” Hon Kiplangat Erick alisema
Haya yanajiri baada ya Rais Ruto kulaani mashambulizi yanayolenga nchi za Ghuba huku akionya kuwa mzozo huo unatishia kusambaratisha amani na usalama wa kimataifa.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Rais amesisitiza umuhimu wa diplomasia katika kusuluhisha migogoro ya kimataifa.
“Ni wazi kuwa kuenea kwa mzozo huu katika eneo zima kunaleta tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa,” amesema Rais Ruto.
Wakati mvutano ukiendelea, ripoti kutoka Wizara ya Ulinzi ya Umoja wa Falme za Kiarabu zinaonyesha kuwa Iran ilirusha makombora 165 ya balestiki, makombora 2 ya cruise na ndege zisizo na rubani 541 kuelekea taifa hilo.
Ingawa mengi yalidunguliwa, baadhi ya makombora zilipiga maeneo muhimu ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zayed na hoteli ya Burj Al Arab.
Nchini Qatar, makombora 66 na ndege zisizo na rubani 12 zilirushwa, huku vipande vya milipuko vikisababisha athari katika maeneo ya viwanda jijini Doha.
Kwa upande wa Kuwait, mamlaka ziliripoti kudungua makombora 97 ya balestiki na ndege zisizo na rubani 283 ndani ya kipindi cha siku mbili. Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuwait na kambi ya kijeshi ya Marekani ya Camp Arifjan, ambapo wanajeshi watatu wa Marekani waliripotiwa kufariki.
Nayo Bahrain imesema ilidungua makombora 61 na ndege zisizo na rubani 34, huku mashambulizi yakisababisha moto mkubwa katika kambi ya Marekani katika Bandari ya Salman pamoja na kuathiri eneo la kibiashara la Seef District.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora imetoa ushauri wa usafiri na usalama kwa Wakenya wanaoishi Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Nje na Diaspora Roselyne Njogu, zaidi ya Wakenya 400,000 wanaishi na kufanya kazi katika mataifa ya Ghuba, jambo linaloongeza wasiwasi kuhusu usalama wao iwapo mzozo huo utaendelea kuongezeka.









