Kampuni ya uchukuzi ya Super Metro imethibitisha tukio lililohusisha moja ya mabasi yake mnamo Februari 24 katika eneo la Kitengela,kaunti ya Kajiado.
Katika taarifa yake tarehe 26 Februari 2026, Kampuni hiyo imeripoti kwamba basi husika, lenye usajili KDK 060H, lilikuwa safarini kutoka Kitengela kuelekea Nairobi likiwa na abiria 32, liliposimamishwa na kundi la waendesha boda boda waliokuwa na ghadhabu wakidai kwamba kondakta wa basi alikuwa amemsukuma abiria kutoka kwenye gari, jambo ambalo liliwashtukiza abiria waliokuwa ndani
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, taarifa za awali zinaonyesha tukio hilo lilisababisha kifo.
Basi hilo kwa sasa linazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Athi River huku dereva na kondakta wakiwa wamekamatwa wakisubiri uchunguzi kukamilika.
“Tunashirikiana kikamilifu na vyombo vya usalama pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) huku uchunguzi kuhusu kisa hiki ukiendelea.”
Awali, familia ya marehemu Joseph Mureithi ilitaka mamlaka kuchukua hatua za haraka, huku mashahidi wakidai kuwa muda mfupi baada ya kushushwa, basi lilimgonga na kuondoka kwa kasi likimuacha akiwa amejeruhiwa vibaya kando ya barabara.
Mmoja wa mashahidi alinukuliwa akisema, “Alipanda basi, na likaondoka. Tulipofika sehemu ya chini, ghasia zilizuka, na kijana huyo akasukumwa kutoka kwenye basi na akaanguka chini. Mwanzoni nilidhani ameumia kidogo tu, lakini tulipofika karibu, kichwa chake kilikuwa kimepasuka.”









