Rais William Ruto amesisitiza kujitolea kwa taifa la Kenya kuimarisha zaidi uhusiano wake wa kibiashara na wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya (EU), akiutaja kuwa soko kubwa zaidi la mauzo ya nje ya nchi na mshirika wake wa kimkakati wa muda mrefu.
Akizungumza baada ya mazungumzo na balozi wa EU nchini Kenya, Henriette Geiger, ikuluni jijini Nairobi Juma nne tarehe 24 Februari 2026 rais Ruto alisema Kenya na EU zina ushirikiano imara wa kibiashara, uwekezaji na maendeleo unaokua kwa kasi.
Rais alisema mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Kenya na EU (EPA), ulioanza kutekelezwa Julai 2024, ulikuwa umefungua ukurasa mpya katika uhusiano wa kibiashara wa pande mbili kwa kuzipa bidhaa za Kenya fursa ya kuingia katika soko la Ulaya bila ushuru wala vizuizi vya kiwango.
“Kupitia mashauriano ya mara kwa mara, tunaendelea kuchunguza njia za kunufaika kikamilifu na fursa zilizo chini ya EPA ya Kenya na EU ili kulinda na kupanua upatikanaji wa bidhaa za Kenya,” alisema Ruto huku akiongeza kuwa lengo la Kenya ni kupanua masoko ya kimataifa kwa wakulima, wajasiriamali na viwanda vyake.
EPA inatarajiwa kunufaisha kwa kiasi kikubwa sekta muhimu za mauzo ya nje kama vile kilimo cha bustani (horticulture), chai, kahawa na mazao mabichi, ambazo kwa muda mrefu zimelitegemea soko la Ulaya.
Kwa kuhakikisha upatikanaji wa soko unaotabirika, mkataba huo unatoa uhakika kwa wauzaji nje na wawekezaji huku ukiimarisha ushindani wa Kenya.
Kiongozi wa taifa zaidi alisisitiza kuwa serikali ya Kenya ililenga kutumia kikamilifu makubaliano hayo kuongeza mapato ya fedha za kigeni, kuchochea ukuaji wa viwanda na kubuni ajira, hasa kwa vijana.
Mkutano huo pia ulitoa fursa ya kupitiwa programu za ushirikiano zilizokuwa zikiendelea pamoja na kuangazia maeneo mapya ya kushirikiana kwa lengo la kuimarisha uthabiti wa uchumi na ukuaji jumuishi.
Kwa kuwa EPA sasa inatekelezwa, maafisa wanatarajia kuongezeka kwa kiwango cha biashara na kuimarika zaidi kwa ushirikiano wa kiuchumi.









