Je wajua kwamba jukumu la kuangazia maslahi ya mwanao sio la mzazi pekee?
Kwa mujibu wa wakili Luka Sawe, jukumu hili pia linajumuisha walimu na jamii kwa jumla kumuangazia mtoto.
Akizungumza katika kipindi cha Hosanna Macheo Jumanne tarehe 24 Februari 2026, Wakili Sawe amewataka wazazi na jamii kuzingatia lishe na huduma za afya za watoto wao pamoja na mahitaji mengine, kwa kuwa haya ni haki wanazopewa na sheria.
Kipindi cha Hosanna Macheo huenda hewani kila Jumatano hadi Ijumaa kwanzia saa kumi na moja hadi saa tatu asubui kikiendeshwa na mwanahabari aliyekolea Victor Mandala kwenye idhaa ya Bibia Husema Broadcasting.
“Mtoto akipata lishe bora anakomaa kiakili na kimwili,” amesema wakili Sawe.
Aidha ameongeza kwamba ni muhimu mtoto kupelekwa hospitalini na kupata huduma za kitaalam anapokuwa mgonjwa bila ya kurejelea mbinu nyingine.
Kando na hayo, wakili Sawe aliwahimiza wazazi kuzingatia elimu ya watoto wao, la sivyo watakabiliwa na mkono wa sheria kwa uzembe.
“Kama kuna mtoto ambaye alifanya mtihani wa kitaifa wa gredi ya tisa na bado hajajiunga na gredi ya 10, unafaa uripoti kwa chifu au kwenye kituo cha polisi kilicho karibu nawe,” amehimiza Sawe.
Wakili Sawe ameongeza: “Ni haki ya mtoto kuendelea na masomo.”
Wakili huyo pia amewatahadharisha walimu dhidi ya kutoa adhabu ya viboko, akieleza kuwa imepigwa marufuku nchini kwa kuwa inakiuka haki za watoto.
“Hadi pale sharia itabadilishwa, wewe mwalimu ujue adhabu ya viboko haipo tena, ni kinyume na sharia,” amesisitiza wakili.
Adhabu ya viboko kwa watoto ni kinyume cha sheria katika mazingira yote, ikiwemo ndani ya familia kwa mujibu wa katiba ya Kenya mwaka 2010.









