Wabunge wamepinga ombi la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) la kutengewa shilingi bilioni 63 kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, wakisisitiza kuwa shilingi bilioni 43 ambazo tayari zimetengwa na Hazina ya Kitaifa zinatosha.
Katika ripoti iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa IEBC, Moses Sunkuli, ameeleza kuwa bajeti hiyo kubwa inalenga kugharamia vipengele muhimu vya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Sunkuli, gharama hizo zinajumuisha mishahara ya maafisa wa uchaguzi itakayogharimu shilingi bilioni 12.4, usajili wa wapiga kura shilingi bilioni 6.9, na ununuzi pamoja na usimamizi wa vifaa vya kielektroniki vya KIEMS vinavyokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 6.2.
Tume hiyo imekadiria kuwa idadi ya wapiga kura ifikapo mwaka 2027 itafikia milioni 28.63, wakiwemo wapiga kura wapya milioni 6.3 kulingana na Sajili ya kitaifa ya idadi ya watu.
Aidha, vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kuongezeka hadi 55,393 kutoka 46,229 vilivyokuwepo mwaka 2022.
IEBC pia imepanga kuendesha usajili endelevu wa wapiga kura, uthibitishaji wa taarifa za wapiga kura miezi sita kabla ya uchaguzi, pamoja na kubadilisha vifaa 45,352 vya KIEMS vilivyozeeka.
Vifaa vingine 14,000 vilivyonunuliwa mwaka 2022 vinapendekezwa kuboreshwa, kila kifaa kikiwa na thamani ya takriban shilingi 175,000.
Mbali na hayo, Tume imeomba shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kununua ardhi na kuanza ujenzi wa Kituo maalum cha Uchaguzi.
Akisisitiza umuhimu wa ufadhili wa kutosha, Sunkuli ameonya kuwa kuchelewa kupitishwa kwa miswada inayohusiana na maandalizi ya uchaguzi kunaweza kuathiri upatikanaji wa huduma na vifaa muhimu.
“Iwapo masuala haya hayatashughulikiwa kwa wakati, wasambazaji wanaweza kusitisha utoaji wa bidhaa na huduma muhimu kwa uendeshaji wa uchaguzi,” Sunkuli alisema.
Hata hivyo, wabunge wamesisitiza kuwa fedha zilizotengwa tayari zinatosha, huku wakiiagiza IEBC kuwasilisha ripoti kuhusu hali ya vifaa vya KIEMS kabla ya kuidhinisha ununuzi.









