Madaktari Mombasa waonywa dhidi ya mgomo kuhusu kusimamishwa kazi kwa Afisa Mtendaji wa Hospitali ya Coast General

0

Serikali ya kaunti ya Mombasa imetoa onyo kali kwa madaktari dhidi ya kuchukua hatua za kugoma, ikionya kuwa kusitishwa kwa huduma za afya kunaweza kuhatarisha maisha ya wananchi.

Akizungumza na wanahabari kaimu waziri wa afya wa kaunti hiyo Dan Manyala, amesema kuwa kuvurugwa kwa huduma za afya kunaweza kuweka maisha ya wananchi hatarini na kusababisha kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika

Onyo hilo linajiri baada ya muungano wa madaktari KMPDU kutoa notisi ya siku saba ya kugoma wakilalamikia kusimamishwa kazi kwa afisa mkuu mtendaji wa Hospitali ya Coast General, Daktari Iqbal Khandwalla.

Kupitia kwa mwenyekiti wa muungano wa madaktari nchini KMPDU, Daktari Abidan Mwachi, madaktari hao wamesema wataanza kususia kutoa  baadhi ya huduma iwapo malalamishi yao hayataangaziwa ndani ya muda walioweka.

Madaktari hao wanataka kuundwa mara moja kwa kamati huru ya uchunguzi kuchunguza madai ya uzembe wa kimatibabu, kuvunjwa kwa bodi ya hospitali kwa kile wanachodai ni kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, pamoja na hatua za kinidhamu dhidi ya Mbunge wa Mvita Mohammed Machele kwa madai ya matamshi ya kikabila na kudhalilisha wahudumu wa afya.

“Tutachukua hatua dhidi ya Mbunge wa Mvita kwa kukiuka Sura ya Sita ya Katiba, na tunatoa notisi ya mgomo.” Mwachi amesema

Hatua ya kusimamishwa kwa Daktari Iqbal Khandwalla mnamo tarehe 22 Februari 2026 ilifuatia hasira za umma kuhusu madai ya uzembe wa kimatibabu uliodaiwa kusababisha kifo cha Ali Kibwana, aliyekuwa mlinzi wa usiku katika ofisi ya mbunge wa Mvita.

Kwa mujibu wa familia, Kibwana alianguka kazini na kupelekwa kwanza katika kliniki ya kibinafsi kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Coast General kwa matibabu maalum.

Mmoja wa wanafamilia alinukuliwa akisema, “Tulikubali damu iliyoganda itolewe ili kuokoa maisha yake, lakini cha kushangaza hospitali iliweka pesa mbele kuliko ubinadamu.”

Katika taarifa yake, serikali ya kaunti ya Mombasa imesema bodi ya hospitali iliamua kumsimamisha kazi Daktari Khandwalla baada ya mkutano maalum uliojadili masuala ya utawala, kuzorota kwa uhusiano kati ya uongozi na washikadau, pamoja na kupungua kwa imani ya umma kwa hospitali hiyo.

Kaunti imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuruhusu uchunguzi kufanyika bila kuingiliwa huku huduma za afya zikiendelea kutolewa kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here