Mjadala kuhusu mtandao haramu wa kusafirisha Wakenya Urusi kupigana vita kule Ukraine wazidi kupamba moto

0

Mjadala kuhusu madai ya kuwepo kwa mtandao wa maafisa wa serikali wanaoshirikiana na madalali kuwasafirisha Wakenya kwenda kupigana katika vita kati ya Urusi na Ukraine umezidi kushika kasi.

Akizungumza katika Bunge la Kitaifa, mnamo tarehe 18 Februari 2026, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah amefichua kuwa uchunguzi wa pamoja wa idara ya ujasusi NIS na idara ya upelelezi DCI umebaini uwepo wa mtandao huo haramu unaohusisha maafisa wa uhamiaji, vyombo vya usalama na baadhi ya maafisa serikalini.

Ichung’wah amesema uchunguzi huo umeonyesha ushirikiano wa maafisa wa uhamiaji, vyombo vya usalama pamoja na baadhi ya watumishi katika balozi za Kenya nje ya nchi.

“Baadhi ya maafisa kwenye wizara ya uhamiaji wanawawezesha wahalifu kuwahadaa Wakenya wasio na hatia ambao huenda hawafahamu mazingira halisi ya kupigana vita nchini Urusi. Kwa hivyo tunazihimiza idara za NIS na DCI kuwabaini maafisa husika.” alisema Ichung’wah.

Aidha, alifichua kuwa zaidi ya Wakenya elfu moja tayari wamesajiliwa kusafiri kwenda Urusi kupigana vita, wengi wao wakivutiwa na ahadi za mishahara minono na uwezekano wa kupata uraia wa kigeni.

Kiongozi huyo wa wengi pia alitoa wito kwa wizara husika na vyombo vya usalama kuwachukulia hatua kali maafisa wote watakaobainika kuhusika na mtandao huo.

“Ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe mara moja dhidi ya maafisa wote watakaopatikana kuhusika katika biashara hii haramu ya kusafirisha raia wetu,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya ujasusi, athari za ushiriki wa Wakenya katika vita hiyo tayari zimeanza kujitokeza.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Wakenya 39 wamelazwa hospitalini wakipokea matibabu, 30 wamerudishwa nchini, huku 28 wakiripotiwa kutokujulikana waliko.

Aidha, takriban Wakenya 89 wanadaiwa kuwa bado wako mstari wa mbele vitani.

Maafisa wa usalama wameonya kuwa hali hiyo inahatarisha maisha ya raia wa Kenya na pia usalama wa taifa, huku uchunguzi ukiendelea kubaini ukubwa kamili wa mtandao huo na waliouhusika.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here