Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Davis Chirchir, amesema serikali imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya mafuriko nchini, hasa katika jiji la Nairobi, huku ikitenga shilingi bilioni nane kuangazia changamoto hiyo.
Akizungumza katika Bunge la Seneti alipokuwa akijibu maswali kuhusu janga la mafuriko yanayosababisha vifo nchini, Chirchir amesema wizara yake imetia saini makubaliano ya ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Nairobi ili kushughulikia swala hilo.
“Tumetia saini makubaliano na serikali ya Kaunti ya Nairobi ili kufanya kazi kwa pamoja na kushughulikia changamoto za mifereji ya maji jijini. Pia tumetenga takriban shilingi bilioni nane kusaidia serikali ya kaunti kukabiliana na changamoto zinazoendelea za mafuriko.”
Haya yanajiri huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikitabiri kuwa mvua kubwa itaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, hali inayoweza kusababisha maafa zaidi.
Wakati huo huo, Waziri Chirchir ametetea mfumo wa utoaji wa faini za papo hapo kwa madereva wanaokiuka sheria za trafiki uliobuniwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA), akisema unasaidia kuongeza nidhamu barabarani.
“Mfumo huu unahakikisha kwamba madereva wanapofahamu kuwa wanafuatiliwa, wanaendesha kwa umakini zaidi na hivyo kutosababisha ajali.”
Matamshi yake yanajiri baada ya mahakama kusitisha utekelezaji wa mfumo huo mpya hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani itakaposikilizwa na kuamuliwa kikamilifu. Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili Shadrack Wambui, ambaye alipinga uhalali wa mfumo huo wa NTSA.
Mahakama pia iliangazia wasiwasi uliotolewa kuhusu uteuzi wa benki moja kupokea malipo ya faini hizo huku ikiamua kuwa benki hiyo sasa itajumuishwa rasmi kama mhusika katika kesi hiyo ili kutoa ufafanuzi kuhusu jukumu lake.
Kadhalika, amewahakikishia wakazi wa Kaunti ya Tharaka Nithi kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa kushughulikia changamoto katika daraja la Nithi, daraja ambalo limehusishwa na ajali nyingi.
“Daraja la Nithi linafanyiwa usanifu upya, na tunalipa kipaumbele kikubwa suala hili. Naibu Rais anatarajiwa kukagua kazi zitakazoanza rasmi katika daraja hilo.”
Aidha, Waziri huyo amethibitisha mipango ya serikali ya kukarabati barabara kuu ya Nairobi–Mombasa, ambayo imekuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu.









