Mpango wa Rais William Ruto wa kuanzisha kikamilifu hazina ya miundombinu (NIF) na kuelekeza mapato yake kwa miradi ya maendeleo umekumbwa na kikwazo cha kisheria baada ya shirika la Katiba Institute kuwasilisha ombi la kupinga kubuniwa kwake.
Kulingana na hati za mahakama, shirika hilo linataka kutolewa kwa amri za kuzuia serikali kutekeleza Sheria hiyo.
Shirika hilo linataka mahakama kuzuia serikali kutumia mapato kutoka kwa ubinafsishaji wa mali ya umma kwa ajili ya hazina hiyo, ikiwa ni pamoja na pesa zinazotarajiwa kutokana na uuzaji wa hisa katika Kampuni ya Usafirishaji wa Mafuta Kenya Pipeline (KPC) na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.
Wakati huo huo, shirika hilo limeeleza kuwa bunge la Seneti lilitengwa katika mchakato wa kutunga sheria, huku sheria hiyo ikiathiri moja kwa moja fedha za kaunti, jambo ambalo ni kinyume na mahitaji ya kikatiba.
“Sheria hii inadhoofisha jukumu la Bunge la usimamizi wa fedha za umma na inatupilia mbali wajibu wa Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB), ambaye amepewa mamlaka kikatiba ya kuidhinisha na kusimamia matumizi ya fedha za umma.” amesema wakili Henry Paul Gichana.
Haya yanajiri baada ya Rais Ruto mnamo tarehe 9 Machi kuweka wazi kuwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) utakuwa mradi wa kwanza kufadhiliwa kupitia hazina hiyo ya Miundombinu, baada ya kuidhinisha sheria hiyo.
Hazina hiyo imekusudiwa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 5 ndani ya miaka 10 kwa ajili ya miradi ya miundombinu nchini.









