Shirikisho la Soka Barani (CAF) limetangaza kubadili ubingwa wa timu ya taifa ya Senegal wa kombe la bara (AFCON) dhidi ya Morocco katika fainali iliyochezwa tarehe 18 mwezi Januri 2026.
Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne tarehe 17 Machi shirikisho badala yake lilitawaza Morocco waliokuwa wapinzani kwenye fainali hiyo kuwa washindi licha ya kulazwa 1-0.
CAF ilisema kuwa Senegal walichukuliwa kama waliojiondoa kwenye mchuano huo baada ya wachezaji wake kuondoka uwanjani na kusalia nje kwa takriban dakika 17 walipoonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa refa Jean Jacques Ndala aliyewapa wenyeji penalti katika dakika za mazidadi kabla ya kurejea na kuendelea na mchuano ambapo Brahim Diaz alipoteza tuta hilo huku Senegal nao wakipata bao la ushindi katika muda nyongeza kupitia Pape Gueye.
Hata hivyo matokeo hayo yametupiliwa mbali, Morocco wakipewa ushindi wa mabao 3-0 kufuatia rufaa waliyokata kupitia shirikisho lao.
Katika uamuzi wake CAF ilieleza kuwa kutokana na hatua ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani walikiuka sheria inayowazuia kufanya hivyo kabla ya mechi kutamatika bila ruhusa ya mwamuzi ambayo adhabu yake ni kubanduliwa na kupoteza mechi hiyo kwa mabao 3-0.
Hata hivyo katika taarifa yake shirikisho la soka la Morocco limedai kuwa nia yake ya kukata rufaa dhidi ya matukio ya mechi hiyo haikukusudia kubadili matokeo ila kutaka kutumika kwa sheria zilizokuwa zikilinda shindano hilo.
“Shirikisho linasisitiza kujitolea kwake kuheshimu sheria, kuhakikisha uwazi katika mfumo shindani, na kudumisha utulivu katika mashindano ya Afrika,”
Hata hivyo mamlaka ya Senegal imesema kuwa itawasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo katika mahakama ya kutatua mizozo ya michezo.
“Shirikisho la soka la Senegal linakashifu uamuzi huu usio wa haki na usiokubalika, ambao unaisababisha soka ya Afrika kukosewa heshima,” ilisema katika taarifa.
Shirikisho hilo lilisema hatua ya kupinga uamuzi huo ni kutetea masuala ya soka ya taifa la Senegal.









