Mahakama imeiagiza tume ya maadili na kukabili ufisadi EACC kumrejeshea Gavana wa Kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya mali yake yote iliyochukuliwa ndani ya siku kumi.Maagizo hayo yanafuatia uamuzi wa mahakama kuu uliotupilia mbali kukamatwa na kushtakiwa kwa Gavana Natembeya kufuatia madai ya ufisadi.
Hakimu Isabella Barasa amesema kuwa serikali haiwezi kuendelea kuzuilia mali ya gavana huyo licha ya kuwepo kwa uamuzi wa mahakama.
“Serikali haiwezi kuendelea kuzuilia mali ya mlalamishi ilhali tayari kuna uamuzi wa mahakama uliotolewa kuhusu suala hili,” amesema Hakimu Isabella.
Katika uamuzi huo, mahakama ilibaini kuwa haki za kikatiba za Natembeya zilikiukwa wakati wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka dhidi yake.
“Haki za kikatiba za mlalamishi zilikiukwa wakati wa kukamatwa na kushtakiwa kwake.” amesema Hakimu Isabella.
Awali, Natembeya alikamatwa na kufikishwa mbele ya Mahakama ya Ufisadi ya Milimani, ambapo alikabiliwa na mashtaka mbalimbali yanayohusiana na ufisadi.
Uchunguzi wa sakata hiyo uliongozwa na idara ya upelelezi DCI kwa ushirikiano na tume ya maadili na kukabili ufisadi EACC vilevile ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma ODPP kufuatia madai ya ufisadi wa takriban shilingi bilioni 1.4








