Kenya hatarini kupoteza AFCON

0
Rais William Ruto (aliyesimama) akishabikia timu ya Harambee stars alipojiunga na mashabiki wa soka uwanjani Kasarani. (awali)

Hatma ya Kenya kuwa mwenyeji wa michuano ya kandanda ya kuwania kombe la bara Afrika (AFCON) 2027 ipo kwenye mizani kutokana na hitaji la kulipa ada ya shilingi bilioni 3.9.

Hili ni hitaji la lazima kwa mwenyeji wa kinyanganyiro hicho kulipa ada hiyo kwa shirikisho la soka barani (CAF) ambalo Kenya inayotarajiwa kuwa mwenyeji mwenza pamoja na Uganda na Tanzania ingali kulitimiza.

Akifika mbele ya kamati ya Michezo na Utamaduni ya bunge la Kitaifa, Alhamisi 19 Machi 2026 katibu wa idara ya michezo Elijah Mwangi, alifichua kuwa CAF ilikuwa imetoa makataa ya hadi mwisho wa mwezi Machi 2026 kwa Kenya kutimiza hitaji hilo ambalo Uganda na Tanzania walikuwa tayari wamekamilisha.

“Tunafahamu kuwa mataifa yetu ya ‘Pamoja’ ambayo ni Uganda na Tanzania yamelipa, ila Kenya ingali kulipa, na hivyo matayarisho ambayo tumefanya ili kuwa mwenyeji wa AFCON yanaweza kuwa hatarini iwapo hatutaweza kutimiza matakwa hayo kufikia tarehe 30 Machi,” alieleza katibu.

Alikuwa akiirai kamati hiyo pamoja na hazina ya kitaifa kuidhinisha bajeti ya ziada ili kuwezesha kuafikia hilo.

Kando na hilo Mwangi pia aliibua hofu mbele kamati hiyo inayoongozwa na Dan Wanyama kuhusu uwezekano wa kukamilika kwa ukarabati wa nyanja za Kasarani na Nyayo ndani ya miezi sita ijayo ilivyohitajika na CAF kama sehemu ya matayarisho.

Alieleza kwamba kampuni iliyopewa kandarasi ya kukarabati uwanja wa kimataifa wa Kasarani ilikuwa imepunguza utendakazi wake kutokana na deni la shilingi bilioni 3.7 huku mkandarasi katika uwanja wa Nyayo akiondoka kazini kutokana na deni la shilingi bilioni 2.7.

Licha ya hili kujiri chini ya mwezi mmoja baada ya kamati hiyo kupinga ombi la wizara ya Michezo la kutaka kuongezewa mgao wa bajeti uliotengewa AFCON, imeahidi kujitolea kuhakikisha upatikanaji wa ada hitajika za kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here