Wizara ya kawi imehakikisha kuwa Kenya ina akiba ya kutosha ya mafuta.
Kwa mujibu wa Katibu katika wizara ya kawi Mohamed Liban, serikali ina akiba ya kutosha licha ya wasiwasi uliopo
Aidha amesema kuwa uhaba unaoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo unasababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta kurundika bidhaa hiyo wakitarajia upungufu kutokana na mzozo unaoendelea katika Mashariki ya Kati.
“Serikali ina akiba ya kutosha ya kuhudumia nchi kwa siku kadhaa. Uhaba unaoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo unasababishwa na baadhi ya wafanyabiashara kurundika mafuta wakitarajia upungufu kutokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati,” Liban amesema.
Liban pia amethibitisha kuwa Kenya imepokea zaidi ya lita milioni 100 za mafuta kufikia tarehe 19 Machi, akisema akiba hiyo inatarajiwa kudumu kwa wiki mbili zijazo.
“Nchi imepokea zaidi ya lita milioni 100 za mafuta kufikia tarehe 19 Machi, na akiba hiyo inatarajiwa kudumu kwa wiki mbili zijazo,” amesema Mohamed Liban.
Kadhalika amehakikisha kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa kawi (EPRA) inashughulikia hali hiyo kikamilifu kuhakikisha kuwa wauzaji wa mafuta wanaanza tena usambazaji wa kawaida wa petroli.
“EPRA kwa sasa inashughulikia ulimbikizaji wa mafuta katika masoko kutokana na matarajio ya kupanda kwa bei.”
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, unaohusisha Marekani, Israel, na Iran, umeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa nishati duniani.
Mashambulizi katika eneo hilo yalisababisha Iran kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia kuu ya baharini ambapo zaidi ya asilimia 20 ya mafuta ghafi duniani na gesi iliyoyeyushwa hupitia.









