Ardhi ni raslimali muhimu inayohitaji usimamizi wa haki

0
Jaji mkuu Martha Koome (kushoto) akiwapongeza makamishna wapya baada ya kuapishwa.

Makamishna saba wapya wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) wameapishwa kuashiria hatua muhimu ya kuimarisha mfumo wa uongozi na usimamizi wa ardhi nchini.

Saba hao ni Dr. Abdillahi Saggaf Alawy, pamoja na Susan Oyatsi, Daniel Murithi Muriungi, Kigen Vincent Cheruiyot, Julie Ouma Oseko, Mohamed Abdi, na Mary Yiane Seneta.

Kuapishwa kwa maafisa hao Jumatatu tarehe 23 Machi 2026 kumeifanya tume hiyo kuwa na idadi hitajika ya makamishna wakijiunga na Esther Mathenge Murugi na Tiyah Galgalo ambao ni makamishna wawili waliokuwa wamesalia.

Akiongoza shughuli hiyo jaji mkuu Martha Koome aliwataka makamishna wapya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwazi na bila upendeleo akisistiza kuwa ardhi ni raslimali nyeti iliyohitaji usimamizi wa haki ili kulinda maslahi ya wananchi.

‘‘Hivi mnavyochukua uongozi wa ofisi hii mnafanya hivyo ndani ya taasisi inayoshikilia nafasi muhimu ya kikatiba nchini kama mtumishi muhimu wa usimamizi wa ardhi.’’ Alisema Koome.

Akizungumza baada ya kuapishwa, mwenyekiti Abdillahi Saggaf Alawy alisisitiza umuhimu wa uangalizi wa ardhi nchini akiahidi kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Ardhi inasalia mojawapo ya raslimali muhimu katika taifa letu. Inaadhiri maisha, maendeleo, uwekezaji, udumishaji wa mazingira na haki ya jamii.’’ Alisema.

“Tunajitolea kutekeleza jukumu letu la kikatiba kwa maadili, utaalamu, uwazi na bila mapendeleo.”

Katika taarifa tume ilisema kuwa uteuzi wa saba hao ulikuwa hatua kubwa katika juhudi zilizokuwa zikiendelea za kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na uangalizi mzuri wa ardhi ya umma.

NLC huwa na jukumu la kusimamia ardhi ya umma, kutadhmini ugavi wa ardhi, na kushughulikia mizozo ya kihistoria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here