Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, amewahakikishia Wakenya kuwa taifa liko tayari kuwa mwenyeji wa Kombe la Taifa Bingwa Barani Afrika (AFCON) 2026, huku akipinga uvumi uliosambaa kwamba Kenya haitaweza kuandaa mashindano hayo.
Akizungumza mbele ya Bunge la Seneti, Waziri Mvurya amesema serikali iko katika harakati za kuhakikisha kuwa malipo ya Shilingi Bilioni 3.9 ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo yanafanywa kwa wakati.
“Wakati Kenya ikijiandaa kwa AFCON, ambayo itaandaliwa pamoja na Uganda na Tanzania, nataka kuwahakikishia Wakenya wote na wadau kwamba tuko tayari,” Mvurya alisema.
Ameongeza, “Tayari tunawasiliana na kamati za bunge na Hazina ya Kitaifa ili kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu. Kenya iko tayari kuandaa AFCON ya kufana.”
Aidha, Waziri Mvurya amebainisha kuwa serikali inajikakamua kuhakikisha kuwa Uwanja wa Michezo wa Talanta unakamilika kwa wakati unaofaa.
Matamshi ya Waziri Mvurya yanajiri siku chache baada ya Rais wa Shirikisho la Soka humu nchini (FKF), Hussein Mohammed, kusisitiza utayari wa kenya kuwa mwenyeji wa kipute cha AFCON.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha habari Jumatatu, Machi 23, 2026, Mohammed amesema nchi ilijifunza kutokana na changamoto zilizokumba maandalizi ya mchuano wa CHAN mwaka jana.
“Wakati wa CHAN, kulikuwa na mashaka mengi kuhusu kama tungeweza kuandaa mashindano hayo, lakini tulithibitisha kuwa tunaweza,” Mohammed alisema.
“Ukizidi kuangalia matukio makubwa ya michezo nchini, kuanzia CHAN hadi Safari Rally na raga ya kimataifa, yote yamekuwa ya kuvutia. Nina imani kwamba nchi ina uwezo wa kuandaa mashindano haya,” aliongeza.









