
Kenya imeteuliwa kuwa mwenyeji wa msururu wa mechi za kimataifa mwaka 2026 kwa wanawake zitakazochezwa kati ya tarehe 11 na 15 Aprili.
Taarifa hii ilitolewa Juma nne tarehe 24 Aprili 2026 na waziri wa Michezo Salim Mvurya aliyetaja hatua hiyo kama upenyo mkubwa kwa mchezo wa kandanda nchini na sekta pana ya michezo.
“Nimefurahi kutangaza kwamba Kenya imeteuliwa kwa mara nyingine kuwa mwenyeji wa mechi za wanawake za FIFA 2026, ikiashiria hatua ya kihistoria taifa letu linapoandaa hafla ya kimataifa ya kandanda kwa mara ya kwanza kabisa,” Mvurya alisema.
Mechi hizo zitakazochezwa katika uwanja wa kimataifa wa Nyayo, zitaleta pamoja mataifa ya India, Australia na Malawi katika hafla ya kihistoria itakayoandikisha mara ya kwanza kwa taifa kuandaa hafla ya kimataifa ya mashindano ya kandanda chini ya shirikisho la soka ulimwenguni FIFA.
Uteuzi huo umeiweka Kenya katika ramani ya kimataifa ya mashindano ya soka kama mwenyeji ikiashiria imani ya FIFA kwa uwezo wa taifa na utayari wake katika kuandaa mashindano ya kimataifa hata inapojiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya bara (AFCON) mwaka ujao.
“Uteuzi huu ni imani dhabiti kwa uwezo ambao Kenya imeonyesha wa kuwa mwenyeji. Unadhibitisha kile ambacho dunia na bara letu imekuwa ikishuhudia kila mara uwezo wa Kenya wa kupangilia, kuandaa kwa ufanisi hafla za michezo yenye hadhi ya kimataifa.’’ Aliongeza Waziri.
Michuano hiyo inatarajiwa kuwapa Harambee Starlets nafasi muhimu ya kushindana na wapinzani mbalimbali wa kimataifa kwenye uwanja wa nyumbani pamoja na kutoa jukwaa la kuonyesha talanta ibuka kwenye kandanda ya akina dada.
Kando na mashindano, hafla hiyo itakuwa ikitumika kama sehemu pana ya juhudi za kuinua kiwango cha Kenya katika michezo ya kimataifa huku serikali ikiangazia uwekezaji unaoendelea katika miundombinu na mageuzi ya sera inayolenga kuimarisha sekta ya michezo.








