Kenya hatua mbele AFCON

0
Rais William Ruto (aliyesimama) akishabikia timu ya Harambee stars alipojiunga na mashabiki wa soka uwanjani Kasarani. (awali)

Waziri wa michezo Salim Mvurya amedhibitisha kuwa serikali imelipa ada ya kuiwezesha Kenya kuwa mwenyeji wa kinyanganyiro cha soka barani Afrika (AFCON) mwaka wa 2027.

Kupitia taarifa Mvurya alisema kuwa shilingi bilioni 3.9 zilizohitajika zilikuwa zimelipwa kwa wakati mwafaka kabla ya tarehe 30 Machi ambayo ilikuwa ndio siku ya mwisho ya kufanya hivyo kwa mujibu wa shirikisho la soka barani (Caf).

“Kwa kutimiza mahitaji serikali imelipa USD milioni 30 (Ksh 3.9 bilion) ada ya kuandaa kwa CAF, kudhibitisha utayari wa Kenya kufanikisha mchuano fanisi wa bara,’’ Waziri alisema.

Taarifa ya waziri Jumanne tarehe 31 Machi 2026 ilijiri wiki mbili baada ya katibu wa Idara ya michezo Elijah Mwangi kufichua kuwa Kenya haikuwa imelipa ada hiyo ya lazima ili kuwa mwenyeji.

Katika taarifa yake ya punde waziri alifichua zaidi mabadiliko katika kamati andalizi ya mchuano huo (LOC).

“Serikali imebuni kamati inayojumuisha washirika mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi kutoka pande zote muhimu za ufanikishaji,” alisema.

Kuhusu masuala ya nyanja na vituo vingine muhimu, Mvurya alitoa hakikisho kuwa serikali itazidisha maradufu juhudi zake kwa kuzingatia masuala yaliyoibuliwa na wakaguzi wa Caf wakati wa ziara yao ya mwisho nchini.

Mkutano baina ya wenyeji wenza wa mchuano huo Kenya, Uganda na Tanzania umeratibiwa mwezi wa Aprili ili kubuni mfumo wa pamoja utakaorahisisha usafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here