Waathiriwa 1,224 wa maandamano waliotambuliwa na KNCHR kwa ajili ya fidia, wahimizwa kuwasilisha ushahidi ifikapo Aprili 3

0

Tume ya Kitaifa ya kutetea Haki za Kibinadamu nchini (KNCHR) kupitia kwa mwenyekiti wake Claris Oganga imetoa taarifa mpya kuhusu maendeleo ya mchakato wa kulipa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Machi 6, 2026, tume imesema kuwa hadi kufikia sasa, imekusanya idadi ya zaidi ya waathiriwa 1,224 wa ukiukaji wa haki za binadamu huku mchakato wa uhakiki ukiendelea.

Tume hiyo aidha imeeleza kuwa idadi hiyo inajumuisha visa mbalimbali, ikiwemo mauaji ya kiholela, mateso, utekaji nyara, ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na wale waliopoteza mali.

Aidha, KNCHR imesema kuwa inashauriana na wadau mbalimbali wakiwemo waathiriwa, asasi za kiraia, na taasisi za serikali kabla ya mchakato wa ushiriki wa umma kuanza

“Tunashauriana na washikadau mbalimbali wakiwemo waathiriwa, asasi za kiraia, na taasisi za serikali kabla ya mchakato wa ushiriki wa umma kuanza,” Claris amesema.

“Hatua hii inatekelezwa kufuatia agizo la Rais William Ruto kupitia notisi ya serikali, ambapo aliitaka KNCHR kuwasilisha ripoti kuhusu mfumo huo ndani ya siku sitini,” Ripoti imesema.

Hata hivyo, tume hiyo imeonya kuwa imekumbwa na changamoto ya kifedha, ikieleza kwamba imeshindwa kufika maeneo mengi nchini kwa sababu ya ukosefu wa fedha, na kuitaka Hazina ya Taifa kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge bila kucheleweshwa.

Wakati huo huo, KNCHR imewahimiza waathiriwa kujitokeza, ikisema waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, wakiwemo walioathirika wakati wa maandamano, wanapaswa kuripoti matukio hayo na kuwasilisha nyaraka muhimu kama vile fomu za P3, ripoti za matibabu, taarifa za polisi, ripoti za uchunguzi wa maiti pamoja na ushahidi mwingine unaohitajika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here