Madina Okot amechaguliwa kujiunga na timu ya Ligi ya Kitaifa ya Wanawake ya Mpira wa Vikapu ya Marekani (WNBA), Atlanta Dream, katika rasimu ya WNBA.
Okot anakuwa mkenya wa kwanza kuchaguliwa katika raundi ya kwanza ya rasimu hiyo.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Okot, ambaye anatoka Mumias, Kenya, alisema hakuweza kufikiria kuwa ndoto yake ingetimia kwa haraka kuliko alivyotarajia.
“Kuwa hapa tu ni jambo kubwa kwangu kwa sababu miaka sita iliyopita sikujiona nikiwa hapa leo. Ndoto yangu ilikuwa kucheza kitaaluma katika WNBA. Sikujua ingechukua miaka sita tu.” Alisema Okot.
Akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 6, Okot, ambaye hivi karibuni alichezea timu ya South Carolina Gamecocks, aliingia kwenye rasimu baada ya msimu mzuri wa 2025/26 uliomfanya kuwa mmoja wa wachezaji bora wa nafasi ya mbele katika mpira wa vikapu wa vyuo vya wanawake.
Madina alikuwa sehemu ya kikosi cha Gamecocks kilichofika fainali ya Mashindano ya Mpira wa Vikapu ya Wanawake ya NCAA Divisheni ya Kwanza, na kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki katika kiwango cha juu zaidi cha mpira wa kikapu wa vyuo vikuu.
Maendeleo ya Okot katika mchezo huu yamekuwa ya haraka sana, kwani alianza kucheza mpira wa kikapu mwaka 2020 pekee.









