Mafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabili Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya NACADA wamenasa shehena kubwa ya kemikali ya Ethanol inayotumiwa kutengeza pombe yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 4 katika mtaa wa Runda jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa NACADA Oparesheni hiyo ilitekelezwa kufuatia taarifa za kijasusi kwa ushirikiano na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru KRA na wenzao wa polisi ambao wamekuwa wakifuatilia pombe hiyo kwa mda.
Kabla ya kunaswa kwa shehena hiyo mshukiwa aliwaelekeza polisi hadi ghala moja kando ya barabara ya Pan Afric ambako walipata jumla ya lita 1,645 za ethanol zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mapipa makubwa ya lita 250 na mitungi ya lita 20 na vifaa vingine.
Akizungumza baada ya Oparesheni hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NACADA Anthony Omerikwa amefichua kuwa wahalifu hao wamebuni mbinu mpya ya kusafirisha pombe haramu.
“Tumegundua kwamba wahalifu hupokea bidhaa hiyo kwa wingi lakini huigawanya katika vipimo vidogo – chupa, mitungi, – ambavyo ni rahisi zaidi kusafirisha bila kugundulika,” Omerikwa alisema.
Omerikwa ametoa onyo kali kwa wanaohusika na biashara hiyo haramu akisisitiza kuwa NACADA haitalegeza Kamba katika juhudi zake katika kukabili matumizi ya pombe na dawa za kulevya humu nchini.
“Nacada haitalegeza Kamba katika kukabili utumizi wa pombe na dawa za kulevya. Tutaendelea kuzilinda familia za Wakenya kutokana na hatari za pombe haramu.” Aliongeza.









