Wananchi Wa Haiti Waandamana Kupinga Kuondoka Kwa Maafisa wa Kenya Nchini Humo

0

Wananchi nchini Haiti wameandamana kupinga kuondoka kwa mafisa wa polisi wa Kenya waliokuwa katika kikosi cha kukabili magenge chini ya mpango wa Multinational Security Support MSS.

Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii waandamanaji walizuia msafara wa maafisa hao kuelekea maeneo ya St. Mark na Pont-Sonde wakielezea kutoridhishwa na uamuzi wa kuwaondoa.

“Hatutaki kuondolewa kwa maafisa wa polisi wa Kenya; wanatusaidia kurejesha usalama.” Wananchi walisikika wakisema.

Vizuizi viliwekwa barabarani huku baadhi ya maafisa wakilazimika kusafirishwa kwa helikopta kutoka maeneo ya Petite Riviere na Pont-Sonde baada ya maandamano kuongezeka.

Kikosi cha mwisho cha maafisa wa polisi wa Kenya kinatarajiwa kurejea nchini hivi karibuni kikihitimisha jukumu lao la kurejesha usalama katika taifa hilo la ukanda wa Caribbea lililokumbwa na machafuko ya magenge.

Kuondoka kwao kunafungua njia kwa kikosi kipya cha kukabili magenge maarufu Gang Suppression Force GSF kilichoidhinishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa mwezi Oktoba mwaka 2025.

Kikosi hicho kipya kitaongozwa na mafisa kutoka Chad huku kundi la Kwanza likiwa tayari limewasili mjini Haiti mapema Mwezi Aprili kuanza Oparesheni ya Kulinda Amani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here