Wahudumu wa afya katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi MTRH Jijini Eldoret wamesitisha mgomo wao uliokuwa uanze leo, kufuatia mazungumzo na uongozi wa hospitali hiyo.
Vyama vya wafanyakazi vilifikia makubaliano na usimamizi wa hospitali kurejea kazini, hatua inayotoa afueni kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu.
“Hati tunayotia saini leo ni ushindi mkubwa kwa wafanyakazi wa MTRH.” Katibu Mkuu wa muungano wa madaktari nchini KMPDU tawi la Kaskazini Mwa Bonde la Ufa, Edward Rono, amesema.
Wahudumu hao wamesema kuwa hatua ya kuitisha mgomo ilitokana na changamoto kadhaa kazini, zikiwemo ukosefu wa bima ya afya, mazingira duni ya kazi, uhaba wa fedha hospitalini miongoni mwa masuala mengine.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Muungano maafisa wa Kliniki KUCO Tawi la Kaskazini mwa Bonde la Ufa Wamalwa Simiyu; amesema kuwa iwapo maswala yaliyoibuliwa hayatatekelezwa basi watafanya mgomo.
“Tunatoa muda wa wiki mbili, na ikiwa matakwa yetu hayatatekelezwa kama yalivyo katika makubaliano haya, maandamano yataanza bila notisi.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa M.T.R.H. Dkt. Philip Kirwa hospitali hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 2 kutoka bima ya mamlaka ya afya ya jamii SHA huku ikisubiri kupokea shilingi bilioni 1 zaidi.
“Mgomo ulipaswa kuanza kesho, hivyo hatujapoteza muda wowote kwani wafanyakazi wanapaswa kurejea kazini mara moja.”









