Msitegemee mtandao kupata taarifa ya nyumbani, rais awaambia wakenya ughaibuni

0

Rais William Ruto amewatahadharisha wakenya wanaoishi nje ya nchi dhidi ya kutegemea mitandao ya kijamii pekee kupata habari za nyumbani kutokana na kuenea kwa taarifa potovu, habari bandia na maudhui ya kupotosha.

Rais alisema ni muhimu kwa wakenya wanaoishi ughaibuni kudhibitisha taarifa wanazopokea, akibainisha kuwa kuna upotoshaji mwingi wa makusudi unaolenga kufanikisha malengo ya kisiasa na binafsi.

Akihutubia wakenya wanaoishi Roma, Italia, Jumatatu tarehe 20 Aprili, kiongozi wa taifa alieleza wasiwasi wake kuhusu juhudi za makusudi za kupotosha kupitia taarifa kwa sababu za kisiasa.

“Ikiwa utaingia mtandaoni leo, unaweza kudhani hakuna jambo jema linaloendelea nchini Kenya. Ninawasihi msitumie mitandao ya kijamii pekee kupata habari kuhusu nyumbani,” Rais Ruto aliambia mkutano huo.

Rais, ambaye yuko katika ziara rasmi nchini Italia, aliwahakikishia waliohudhuria kuwa ajenda ya serikali ya kuibadilisha Kenya kuwa taifa la uchumi wa kiwango cha juu inaendelea licha ya upinzani mkali kutoka kwa wakosoaji.

“Lengo langu si uchaguzi mkuu ujao. Ninalenga kuibadilisha Kenya,” alisema rais.

Aliongeza kuwa ajenda ya mabadiliko ya nchi ilikuwa imecheleweshwa kwa muda mrefu kutokana na uongozi duni, akisema ameazimia kufanya maamuzi magumu yatakayoipeleka nchi katika hatua inayofuata.

Rais Ruto aliwaambia waliohudhuria kuwa usimamizi wa uchumi wa serikali yake umefanikiwa kuokoa Kenya dhidi ya kushindwa kulipa madeni yake hata baada ya kutambuliwa kuwa katika hatari kubwa.

Rais alihusisha mafanikio hayo na nidhamu ya kifedha ya serikali pamoja na maamuzi magumu yaliyosaidia kuilinda nchi dhidi ya mgogoro wa kiuchumi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here