Murkomen Akanusha Madai ya Unyakuzi wa Ardhi ya Bilioni 20 Runda, Aagiza Uchunguzi

0

Waziri wa Usalama na maswala ya Ndani ya Nchi, Kipchumba Murkomen, amepuuzilia mbali madai yanayosambaa kuhusu kuhusika kwake katika unyakuzi wa ardhi ya ekari 300 katika eneo la Runda, Kaunti ya Kiambu, inayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 20.

Kupitia taarifa iliyotolewa na mkuu wa mawasiliano katika ofisi yake, Julius Sigei, Murkomen amesema hana ufahamu wowote kuhusu ardhi hiyo na hana nia ya kuinyakua.

“Sina ufahamu wowote kuhusu ardhi inayozungumziwa, wala sina nia yoyote ya kuinyakua.” Murkomen amesema.

Aidha, amekanusha madai kwamba ametumia mamlaka yake kuagiza ulinzi wa polisi katika ardhi hiyo.

Murkomen sasa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pamoja na asasi za uchunguzi kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa kwa kina kuhusiana na madai hayo.

“Ninatoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na kutoa ukweli kuhusu madai haya.” Murkomen amesema.

Taarifa yake imetokana na malalamishi yaliyowasilishwa mahakamani na Daniel Mwangi Mbugua na bintiye Wanjiru Mwangi ambao wameitaka tume ya maadili na kukabili ufisadi EACC kumchunguza Waziri Murkomen, Mbunge wa Kapseret Osar Sudi na mwenzake wa Gatundu Kaskazini Elijah Kururia kwa kuhusika na unyakuzi wa ardhi hyo

Mlalamishi Mwangi ambaye ni mwanawe Mfanyibiashara maarufu Marehemu Mbugua Mwangi ambaye alifariki dunia mwaka 2008 na aliyemiliki ardhi hiyo ameiambia mahakama kwamba Murkomen na wabunge hao wawili wamekuwa wakitumia mamlaka vibaya kuwalinda zaidi ya watu 200 ambao wamevamia ardhi hiyo kinyume na sheria, huku akidai baadhi ya maafisa wa polisi wanahusika katika kulinda uvamizi huo.

Pia amelalamika kuwa sehemu ya ardhi hiyo imehamishiwa kwenye umiliki wa kampuni kwa jina Pamat Enterprise.

Licha ya Murkomen kusema kuwa hana ufahamu kuhusu ardhi hiyo mlalamishi anadai kuwa yeye mwenyewe alimwona waziri huyo katika ardhi hiyo mnamo tarehe 11 Aprili 2026 akiwa kwenye msafara wa magari sita.

Mahakama imeagiza kesi hiyo kutajwa tena tarehe 19 Mei 2026.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here