Waziri wa Afya Aden Duale amewakosoa viongozi wanaodai kwamba Mamlaka ya Afya ya Jamii SHA haifanyi kazi akifichua kuwa baadhi yao ndio wanaonufaika pakubwa kutokana na bima hiyo.
Duale amesema bima hio inagharamia maibabu ya baadhi ya viongozi wa upinzani ambao walihudumu katika ngazi za juu serikalini.
“Viongozi wote nchini, wa sasa na wale walio staafu, ni wanachama wa SHA, wakiwemo wale wanaosema sasa kwamba SHA haifanyi kazi.” Amesema Duale.
Katika kauli ambayo inaonekana kulenga Naibu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka ambae hapo awali ameelezea ati ati kuhusu bima hio, Duale amesema mbali na wakuu hao wa zamani, wapendwa wao pia wanagharamiwa matibabu na SHA.
“Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja ,mamake na mke wake wako chini SHA, Kalonzo Musyoka na Mkewe wanalindwa na SHA sawia Moody Awuori na Mke wake.” Duale amewaambia maseneta.
Aidha amesema kuwa ulaghai kwenye bima ya afya ya jamii SHA umepungua kutoka asilimia 26 hadi asilimia 6 huku akifichua kuwa zaidi ya vituo 1,200 vya afya vimefungwa, huku watu 18 wakifikishwa mahakamani kufuatia uchunguzi unaoendelea dhidi ya wanaofuja fedha za SHA.
“Tangia Aprili mwaka jana nilipoingia katika Wizara hii ya Afya, kiwango cha ulaghai kilikuwa asilimia 26. Sasa nataka kuthibitishia nchi kwamba kutokana na hatua tulizochukua, tuko sasa katika asilimia 6. Tumefunga zaidi ya vituo 1,200 vya afya.” Amesema Duale.
“Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amepokea zaidi ya faili 24, ambapo 18 kati yake, ikiwemo wakurugenzi wakuu wawili wa zamani wa SHA na NHIF, wamefikishwa mahakamani.” Ameongeza Waziri Duale.
Wakati uo huo, amefichua kuwa mpango wa bima ya afya ya EduAfya, ambao awali ulifadhiliwa kikamilifu na serikali, unamadeni kubwa kutokana na bili za hospitali ambazo hazijalipwa wakati wa kipindi cha mpito kutoka Bima ya zamani ya NHIF.
Hata hivyo, ameihakikishia Bunge kuwa fedha zinazohitajika tayari zimetengwa na Serikali ili kulipa madeni hayo yaliyosalia.
“EduAfya awali ilifadhiliwa na serikali na imeacha deni kubwa kwa sababu serikali haikulipa wakati wa kipindi cha mpito.” ameongeza Duale.









