Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amedhibitisha utayari wa bunge kushughulikia masuala yanayoibuliwa na viongozi wa dini.
Alipokuwa mwenyeji wa askofu wa kanisa Katoliki Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria, spika Wetangula alitambua kuwepo kwa hali ya kukata tamaa ndani ya kanisa kutokana na kile kinachoonekana kama ucheleweshaji wa serikali kushughulikia changamoto za kitaifa.
Akizungumza baada ya kikao cha majadiliano kilichofanyika Jumatano asubuhi tarehe 22 Aprili, Wetang’ula ameliomba kanisa kutokuwa na uegemezi katika ukosoaji wake wa masuala ya kijamii na kuambatanisha hoja zake na suluhisho za vitendo.
“Asubuhi hii, wakati wa kikao cha majadiliano na askofu mkuu wa kanisa Katoliki dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria, nililihimiza kanisa kubaki na uwiano katika ukosoaji wake wa masuala ya kijamii na kutoa suluhisho za vitendo,” alisema Wetang’ula katika taarifa.
Aliongeza kuwa bunge linaendelea kujitolea kushirikiana kwa njia ya kujenga na taasisi za kidini, akibainisha kuwa kanisa lina jukumu muhimu katika kuelekeza mjadala wa umma na kukuza mshikamano wa kijamii.
Askofu Muheria, katika hotuba yake, alisisitiza msaada endelevu wa kiroho wa kanisa kwa taifa, akisema viongozi wa dini wanaendelea kujitolea kuliombea taifa na kuhamasisha amani na utulivu ndani na nje ya nchi.
Mkutano huo umefanyika wakati ambapo taasisi za kidini zimekuwa zikikosoa hali ya utawala, kupanda kwa gharama ya maisha, na changamoto pana za kijamii na kiuchumi zinazowakabili wananchi.
Katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa dini nchini wamekuwa wakitoa wito wa uwajibikaji zaidi, uwazi, na mwitikio wa haraka kutoka kwa taasisi za umma.









