Ruto Ampiku Uhuru Kenyatta Kwa Matumizi Ya Fedha

0

Gharama za uendeshaji wa Urais zimezua mjadala mkali baada ya kubainika kuwa ifikapo mwezi Juni, utawala wa Rais Ruto utakuwa umetumia takriban shilingi bilioni 100.

Kiasi hicho kinajumuisha matumizi ya Ikulu, Ofisi ya Naibu wa Rais, pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, Utumishi wa Umma na wizara mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Fedha, Mdhibiti wa Bajeti Dr. Margaret Nyakang’o na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, matumizi ya ofisi ya Urais chini ya Rais Ruto yamefikia shilingi bilioni 88.8 katika kipindi cha chini ya miaka mine karibu sawa na shilingi bilioni 89.9 zilizotumika katika miaka yote 10 ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Hii ina maana kuwa ndani ya kipindi cha takriban miaka minne pekee, matumizi ya sasa yamekaribia, na hata kuvuka, yale ya muhula mzima wa Rais wa awali.

Katika kipindi cha miaka 10, Kenyatta alitumia shilingi bilioni 36.27 katika muhula wake wa kwanza na shilingi bilioni 53.72 katika muhula wake wa pili.

Hata hivyo, serikali imesisitiza kuwa matumizi hayo yanahusisha shughuli muhimu za kitaifa, ikiwemo uendeshaji wa ofisi za juu serikalini na utekelezaji wa majukumu ya kikatiba ya urais.

Bajeti imepanda kutoka asilimia 0.44 ya bajeti ya taifa mwaka wa kifedha 2021/22 hadi asilimia 0.77 ya bajeti ya sasa ya shilingi trilioni 4.2.

Katika kipindi cha miaka mitatu na miezi tisa ya utawala wa Ruto, asilimia 93.7 ya matumizi yote sawa na shilingi bilioni 83 yameelekezwa katika matumizi ya kawaida kama mishahara, safari, mafuta na shughuli za kiutawala.

Hali hii imeibua mjadala kuhusu matumizi makubwa ya fedha katika shughuli zisizo za maendeleo.

Ikulu imeongoza kwa matumizi makubwa zaidi, ikitumia shilingi bilioni 36.3, ikifuatiwa na Afisi ya Utendaji ya Rais iliyotumia shilingi bilioni 35.1.

Ofisi ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki imetumia shilingi bilioni 12.5, huku Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ikitumia shilingi bilioni 3.3.

Katika mwaka huu wa kifedha, bajeti ya Urais imeongezwa hadi shilingi bilioni 32.2 kupitia marekebisho ya bajeti, huku Ikulu ikiongezewa shilingi bilioni 8.9.

Mishahara ya wafanyakazi wa Ikulu pekee inagharimu shilingi bilioni 3.6

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here