Rigathi Gachagua ameondoa ombi lake la kuomba kurejeshwa katika wadhifa wa Naibu wa Rais, katika mabadiliko mapya kwenye kesi ya kungatuliwa kwake afisini.
Hatua hiyo mpya imethibitishwa na mawakili wake ambao wamesema kuwa badala yake, kiongozi huyo wa Chama cha DCP sasa anasaka fidia kufuatia kung’atuliwa kwake madarakani.
Akizungumza wakati wa kusikilizwa wa kesi ya hio katika Mahakama za Milimani, wakili Paul Muite ameiambia mahakama kuwa anataka kulipwa mishahara ambayo angepokea iwapo angeendelea kuhudumu pamoja na fidia ya hasara kutokana na kile amedai ni kungatuliwa kwake kinyume cha sharia.
“Mlalamishi ameacha ombi la kurejeshwa katika wadhifa wa Naibu wa Rais,” wakili Paul Muite ameiambia jopo la majaji watatu lililojumuisha Majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Fred Mugambi.
Wakili Muite aidha amesema mchakato huo uliharakishwa na haukutoa fursa ya haki kwa mteja wake kujitetea kikamilifu.
“Mchakato mzima ulifanywa na Bunge la Kitaifa hadi Seneti kwa kasi ya ajabu. Swali linalojitokeza ni kwa nini kulikuwa na haraka hiyo?”
Kwa upande wake, wakili Elisha Ongoya amesema mchakato huo ulionyesha wazi uvunjaji wa sheria katika namna kesi hiyo ilivyoendeshwa.
“Hata baada ya Spika kusema kuwa kuna muda hadi Jumamosi, muda huo haukuangaziwa licha ya Spika kusema hivyo. Maseneta walipiga kura kumnyima Naibu Rais manufaa ya siku hizo mbili au tatu bila kutoa sababu yoyote.”
Mahakama hiyo ilieleza kuwa ilikuwa imepanga kusikiliza hoja hiyo kwa siku tatu mfululizo, hata hivyo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, usikilizaji hautaendelea kesho na kesho kutwa kama ilivyoratibiwa awali.









