Wizara ya Afya, Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) pamoja na Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) zimefikia makubaliano kufuatia mvutano uliokuwepo kuhusu utekelezaji wa bima ya afya ya SHA kwa walimu kote nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano wa kina uliowaleta pamoja wadau wakuu katika sekta ya afya na elimu, ambapo pande zote zimekubaliana kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za afya kwa walimu na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiibuka tangu kuanzishwa kwa mpango huo.
Aidha, wameafikiana kuhusu masuala sita muhimu yatakayolenga moja kwa moja kushughulikia malalamishi ya walimu kuhusu upatikanaji na ubora wa huduma chini ya bima ya SHA.
Miongoni mwa mabadiliko yaliyotangazwa ni pamoja na kuanzishwa kwa malipo ya shilingi laki tatu kwa familia ya mwalimu atakayefariki, hatua inayolenga kutoa afueni kwa familia za walimu wanaopoteza maisha wakiwa kazini.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari SHA imesema, “mfumo maalum umewekwa kusaidia walimu wanaokumbwa na gharama kubwa za matibabu zinazozidi kiwango kilichowekwa na bima, ili kuhakikisha hakuna mwalimu anayekosa huduma muhimu kwa sababu ya gharama.”
Vilevile, makubaliano hayo yamejumuisha kuwezesha matibabu ya nje ya nchi kwa walimu wanaohitaji huduma maalum na za hali ya juu, katika vituo teule vilivyothibitishwa. Katika hatua nyingine muhimu, Wizara ya Afya, SHA na KNUT zimekubaliana kuondoa mara moja vizuizi vya ushuru na taratibu zilizokuwa zikisababisha walimu kulazimika kulipia huduma za afya kutoka mifukoni mwao.
Aidha, imeelekezwa kuwa vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma chini ya SHA haviruhusiwi tena kutoza walimu malipo ya ziada, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.
Sambamba na hayo, miundo ya usimamizi wa SHA katika ngazi ya kaunti itafufuliwa na kuimarishwa ili kuhakikisha changamoto zinazowakumba walimu zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi katika maeneo yao.
Hatua hiyo ikilenga kuboresha mawasiliano kati ya walimu na watoa huduma za afya.
Hatua hizi zinatarajiwa kurejesha Imani ya walimu katika mpango wao mpya wa afya ya SHA na kuboresha kwa kiasi kikubwa ustawi wao, hali ambayo itachangia pia kuimarisha sekta ya elimu nchini.









