Ruto Asema Hajatalakiana na Eneo la Mlima Kenya.

0

Ubabe wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya unaendelea kushamiri, huku mamia ya viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Kirinyaga wakizuru Ikulu ya Nairobi, ambapo Rais William Ruto ameendelea kusisitiza kuwa yeye ni mshirika mkuu wa eneo hilo na kupuuzilia mbali tetesi za kutengana na wakazi wake.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais amepinga madai yanayoenezwa na kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, kwamba wakazi wa Mlima Kenya wamejitenga na utawala wake.

Rais pia ameeleza kuwa serikali imechukua hatua kali dhidi ya maafisa matapeli katika sekta ya kilimo, katika kile kinachoonekana kumlenga Waziri wa zamani wa Kilimo Mithika Linturi, Rais amesema maafisa hao walikuwa wakitumia nyadhfa zao kujifaidi.

“Wale walikuwa wanatuibia mpaka wanatuibia mbolea si mliskia kun ahata mwengine alikuwa anatuuzia mawe, nilimpatia kazi mahali fulani badala ya kuenda kuwapa wananchi mbolea akaenda akasiaga mawe akaweka kwa magunia anajaribu kupatia wananchi. ” Rais amesema

Kadhalika, Rais ametetea rekodi ya utendakazi wa serikali yake tangu alipoingia madarakani mwaka 2022, akitaja mafanikio katika sekta ya elimu pamoja na juhudi za kuziba pengo katika mtaala wa Elimu ya Umilisi (CBC).

“Wazazi wengi walikuwa wanalalamika hii CBC tunafanyishwa kazi usiku watoto wanasema tumeambiwa tutengeneze gari shuleni, kata box fanya hii, hatukua na walimu wa kutosha, tulikuwa na upungufu wa walimu elfu 116, tulikuwa na shida na madarasa, mimi niliwaambia nitanyorosha maneno. ” Ameongeza Ruto.

Wakati huo huo, ametangaza mpango wa kuongeza shilingi bilioni 2 zaidi katika Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu (NIF), kufuatia Hazina ya Taifa kupokea shilingi bilioni 103.45 kutokana na uuzaji wa sehemu ya hisa za kampuni ya Kenya Pipeline.

Amesema fedha hizo zitatumika kama mtaji wa kuanzisha na kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na ujenzi wa mabwawa makubwa 50.

Miongoni mwa miradi iliyopangwa ni upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, ambapo zabuni tayari zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ikiwemo barabara ya kupaa na kutua ndege, huku ujenzi ukitarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here