Maafisa wakuu wa kaunti ya Mandera wamehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja gerezani kwa kukiuka amri ya mahakama ya kulipa shilingi milioni 11.7 katika mzozo wa fidia ya ardhi.
Mahakama ya mazingira na ardhi ya Garissa ilitoa uamuzi huo Jumanne tarehe 28 Aprili 2026 bila uwepo wa waziri wa Fedha wa kaunti, na katibu, ambao walikuwa wameshtakiwa kwa kukiuka amri ya mahakama.
Kesi hiyo inahusu kipande cha ardhi ambacho serikali ya kaunti ilibainika kukimiliki na kukiendeleza kinyume cha sheria kwa kujenga chuo cha ufundi bila kufuata taratibu sahihi za umilikishaji.
Mahakama hapo awali ilikuwa imeamuru serikali ya kaunti ya Mandera iondoke kwenye ardhi hiyo au imlipe mmiliki fidia, na hivyo kupelekea kutolewa kwa fidia ya shilingi 11,730,733.33.
Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa licha ya maagizo hayo, kaunti haikulipa kiasi hicho wala kuweka fedha mahakamani ndani ya muda uliotolewa.
“Baada ya kushindwa kutii amri za mahakama, wahusika wanahukumiwa wakiwa hawapo mahakamani kifungo cha mwezi mmoja gerezani,” mahakama iliamua.
Jaji pia alitoa amri ya kukamatwa kwa wawili hao, akiamuru wakamatwe na kuwekwa kizuizini.
Wakili wa mlalamishi, alikaribisha uamuzi huo akisema unaimarisha mamlaka ya mahakama na kulinda haki za umiliki wa mali kesi hiyo ikiratibiwa kutajwa tena tarehe 4 Juni 2026.









