Mahakama kuu imetupilia mbali ombi la kikatiba lililokuwa linapinga agizo la Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) la kuyataka magari ya uchukuzi wa umma (PSV) kuondoa graffiti, michoro ya mapambo na vioo vyenye rangi nyeusi, hatua ambayo imekuwa pigo kubwa kwa wahudumu wa matatu wanaotetea utamaduni maarufu ‘nganya culture’ nchini Kenya.
Katika uamuzi uliotolewa Jumatano tarehe 29 Aprili, Jaji Bahati Mwamuye alidumisha uhalali wa notisi ya utekelezaji iliyotolewa na NTSA Mei 2025, akisema agizo hilo lilikuwa halali na muhimu katika kuimarisha usalama barabarani na uzingatiaji sheria katika sekta ya usafiri wa umma.
Ombi hilo lilikuwa limewasilishwa na Michael Makubo, aliyedai kuwa agizo hilo lililenga visivyo wahudumu wa matatu na kuhatarisha utamaduni wa ‘nganya’ ambao ulitajwa kuwa utambulisho wa kipekee wa usafiri wa mijini unaojulikana kwa michoro ya rangi, taa za neon, vioo vyenye rangi nyeusi, mifumo ya burudani yenye sauti kubwa na mapambo ya ndani yaliyoboreshwa.
Makubo alidai kuwa agizo hilo lilikiuka ulinzi wa kikatiba, lilianzishwa bila ushirikishwaji wa kutosha wa umma, na lilikuwa la kibaguzi dhidi ya wahudumu wanaotegemea uboreshaji wa magari kwa ajili ya mvuto wa kibiashara.
“Mlalamishi ameshindwa kuthibitisha ukiukwaji wowote wa haki za kikatiba, kwake binafsi au kwa kundi alilodai kuwakilisha.” Alibaini jaji katika uamuzi.
Jaji alishikilia kuwa vikwazo vya marekebisho ya magari vilithibitishwa chini ya ibara ya 24 ya katiba, inayoruhusu kuwekwa mipaka ya haki pale ambapo usalama wa umma unahusika.
Alibainisha kuwa wajibu wa serikali kuhakikisha usalama barabarani unazidi madai kwamba magari ya uchukuzi wa umma yaliyopambwa ni aina ya uelezaji wa kisanii na kitamaduni unaolindwa.
Mahakama ilifahamishwa kuwa NTSA ilikuwa imewaagiza wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma yaliyo na graffiti, vioo vyenye rangi nyeusi na marekebisho mengine kama hayo kuondoa au kuchukuliwa hatua za kisheria.
NTSA ilitetea notisi hiyo, ikisema hatua hiyo inalenga kuboresha mwonekano kwa abiria na vyombo vya usalama, kuimarisha usalama barabarani na kuhakikisha viwango vinavyofanana katika sekta ya uchukuzi wa umma.
Jaji Mwamuye alikubaliana na hoja hiyo, akisema kuwa notisi hiyo haikuwa sheria mpya bali ukumbusho wa kiutawala wa wajibu ambao tayari umewekwa chini ya kanuni zilizopo za usafiri.









