Katibu Mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna, amepuzilia mbali madai kuwa anatumiwa kuvuruga chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, akisisitiza kuwa yeye ni mwanachama mwaminifu wa muda mrefu wa chama hicho.
Sifuna amesema msimamo wake unatokana na maslahi ya chama na wananchi, akiongeza kuwa madai ya kuwa anahujumu chama hayana msingi wowote.
“Mimi ndio navurugwa kwa sababu shida sio Sifuna wale wanasema tunavuruga chama huo ni uongo mimi sijajua chama kingine tangia niingie kwa maswala ya siasa. ” Amesema Sifuna.
Wakati uo huo, amedai kuwa Rais William Ruto alianza kukiuka makubaliano ya kisiasa kati yake na hayati Raila Odinga hata kabla ya kifo chake.
Ametaja visa vya vifo vya vijana wakati wa maandamano pamoja na kifo cha mwalimu Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi kuwa baadhi ya ishara za ukiukaji wa makubaliano hayo.
“Changamoto zangu zilianza siku nilipotangaza kuwa mkataba huo umekufa, kwa sababu tulikuwa tumekubaliana kuona kukoma kwa utekaji nyara, kusitishwa kwa mauaji ya kiholela, kuheshimiwa kwa vyama vya kisiasa, pamoja na kuheshimiwa kwa ugatuzi na mambo mengine tuliyoorodhesha.” Sifuna amesema.
Sifuna pia amefichua kuwa aliwahi kufikiria kujiuzulu ili kupunguza mvutano ndani ya chama, lakini alishauriwa kinyume na Oburu Oginga.
“Nilimuuliza mheshimiwa Oburu kama bado anaamini sifai kuwa Katibu Mkuu, na nikamweleza niko tayari kujiuzulu ili chama kipate mtu watakayefanya naye kazi kwa urahisi. Lakini alinijibu kuwa hayo ni mambo yaliyopita na akanitaka tushirikiane kuvuka kipindi hiki kigumu.” Sifuna amebainisha.
Sifuna alitimuliwa kutoka wadhfa wa Katibu Mkuu wa ODM akikabiliwa na madai ya kukiuka maazimio ya chama hicho.
Hata hivyo amepatta afueni ya muda baada ya Kamati ya Kutatua Migogoro ya Vyama Vya Kisiasa (PPDT) kusitisha kuondolewa kwake afisini na badala yake kuagiza chama cha ODM kutatua migogoro kupitia asasi za chama.









