Polisi Watumwa Kudhibiti Usalama Katika Barabara ya Mwingi-Garissa

0

Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imetuma kikosi maalum cha maafisa wa usalama kutoa ulinzi kwa magari na abiria katika barabara ya Mwingi–Garissa kufuatia maandamano ya wakazi wanaolalamikia mauaji ya watu wanane yanayodaiwa kuhusishwa na wafugaji wa ngamia.

Katika taarifa, kupitia msemaji wake Muchiri Nyaga NPS imesema: “Tumetuma vikosi maalum kuandamana na magari katika barabara ya Mwingi–Garissa na kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara hiyo.”

Maandamano hayo pia yalichochewa zaidi na mauaji ya mvulana mwenye umri wa miaka 14 kwa jina Joseph Mutemi mwanafunzi wa shule ya msingi ya Kathungu kwenye kaunti ya Kitui alipokuwa akichunga mifugo, mauaji yanayohusishwa na wafugaji wa ngamia.

Maandamano hayo yalitatiza pakubwa safari za magari baina ya Nairobi na maeneo hayo ya Garissa na Mwingi huku baadhi ya abiria wakikwama njiani na kwenye vituo vya mabasi.

NPS aidha imesema kwamba inazifuatilia taarifa muhimu likinuia kuwanasa washukiwa wa mavamizi hayo.

“Tunatambua hofu na wasiwasi uliosababishwa na matukio haya miongoni mwa wakazi. Hata hivyo, tunasisitiza kuwa haya ni matukio ya uhalifu yaliyotekelezwa na watu wachache ndani ya jamii.” NPS imewahakikishia wakazi.

Kwa upande wao Wakazi wameendelea kulaani mauaji hayo na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka.

“Vita iko hapa mpakani na hakuna hatua madhubuti inayochukuliwa. Serikali inajenga vituo vya polisi lakini vinavamiwa na kuharibiwa, watu wanauawa kila siku sasa tuende wapi?” Mmoja wa wakazi alisema.

“Tunamtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, aangalie kwa makini matukio haya na kuhakikisha wahusika wanakamatwa ili tujue sababu ya mauaji ya watu wetu.” Mkazi mwingine aliongeza:

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here