Askofu Omae kumrithi kasisi Kobia NCIC

0
Askofu Kepha Omae (awali) akiwa mbele ya kamati ya bunge kusailiwa.

Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa wanachama wanane waliopendekezwa kuhudumu katika Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), inayohusika na kuhimiza umoja na mshikamano wa kitaifa.

Uidhinishaji huo ulifanyika wakati wa kikao cha bunge siku ya Jumatano, Aprili 29, 2026, baada ya wabunge kupitisha ripoti ya kamati ya Uwiano wa Kitaifa na Fursa Sawa.

Kamati hiyo ilipendekeza kuidhinishwa kwa wateule wote kufuatia mchakato wa uhakiki uliotathmini ufaafu wao kwa nyadhifa hizo.

Dkt. Kepha Omae aliidhinishwa kuwa mwenyekiti wa tume hiyo, pamoja na Josephine Eragae, Joseph Nguyo, Jackson Kedogo, Dkt. Samuel Mwachiro, Irene Tulel, Hassan Ahmed, na Jerusah Mwaathime kama wanachama.

Uteuzi wao unafuatia kumalizika kwa muhula wa kuhudumu wa muda wa miaka sita usioweza kuongezwa wa makamishna wanaoondoka, akiwemo aliyekuwa mwenyekiti, Samuel Kobia, pamoja na makamishna wengine saba, ambao muhula wao uliisha Novemba 17, 2025.

Mchakato wa uhakiki uliongozwa na naibu mwenyekiti wa kamati hiyo, Duncan Mathenge, ambaye ni mbunge wa eneo bunge la Nyeri mjini.

Akiwasilisha hoja ya kupitishwa kwa ripoti hiyo, Mathenge aliambia bunge kuwa wateule wote walikidhi mahitaji ya kisheria na walionyesha uwezo wa kutekeleza majukumu ya tume kwa ufanisi.

“Kamati imeridhika kuwa wateule wana sifa stahiki na wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema.

Baadaye wabunge walijadili na kupitisha ripoti hiyo, wakitambua jukumu muhimu la NCIC katika kuimarisha kuishi kwa amani katika jamii yenye utofauti.

Tume hiyo ilianzishwa baada ya vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007–2008 nchini Kenya, na ina jukumu la kukuza mshikamano wa kitaifa, kuondoa ubaguzi wa kikabila, na kushauri kuhusu sera zinazokuza umoja.

Baada ya kuidhinishwa na bunge, wanane hao sasa wanatarajiwa kuteuliwa rasmi na rais kupitia tangazo la gazeti rasmi la serikali kabla ya kuapishwa kuanza majukumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here