Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya vijana wako tayari kushiriki katika vitendo vya ufisadi iwapo watapata fursa.
Haya ni kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC Abdi Mohamud, ambaye amesema hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa kwa mustakabali wa taifa.
Mohamud aidha amesisitiza umuhimu wa Wakenya kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi.
“Vijana wetu waliulizwa iwapo wangepewa nafasi au fursa ya kujihusisha na ufisadi, je, wangechukua hiyo fursa au la? Cha kushangaza ni kwamba asilimia 80 wamesema wakipewa fursa watajihusisha na ufisadi.” Mohamud amesema.
Wakati uo huo, amekanusha madai kuwa tume hiyo inatumika kisiasa kuwaandama wanasiasa wanaoikosoa serikali, akisisitiza uhuru wake.
“Tume hii ni huru na hakuna haja yetu kutumika na wanasiasa kwani kazi zetu zinaongozwa na sheria na Katiba. Sisi tumechukua kiapo cha kufanya kazi yetu bila uwoga na bila mapendeleo, kwa hivyo serikali yoyote ikikuja hatubagui wala hatuegemei upande wowote.” Mohamud ameongeza.
Aidha, ameizungumzia sakata ya ufisadi inayomhusisha Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, akisema kesi hiyo bado inaendelea.
Amedai kuwa baadhi ya wanasiasa waliwachochea vijana kuharibu mali ya tume hiyo wakati maafisa wa EACC walipokuwa wakifanya upekuzi katika makazi ya gavana huyo mjini Kitale.









