Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga nchini imeonya kwamba Mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia leo hadi Mei 11.
Katika utabiri wake wa hivi punde Idara hiyo imetangaza kwamba mvua itaendelea kunyesha katika Nyanda za juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Pwani, Nyanda za chini Kusini Mashariki, Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki.
“Mvua inatarajiwa kuendelea katika Nyanda za juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Pwani, Nyanda za chini Kusini Mashariki, Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ” imesema Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga.
Aidha imeonya kuwa matukio ya mvua kubwa yanaweza kutokea katika baadhi ya maeneo na kuongeza hatari ya mafuriko.
Kaunti za Nairobi, Kiambu, Murang’a, Nyeri, Embu, Meru, Kirinyaga, na Tharaka-Nithi, ni miongoni mwa kaunti zitakazoshuhudia mvua kubwa pamoja na Kakamega, Bungoma, Vihiga, Siaya, Busia, na Nandi, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, na Nyamira vilevile Nakuru, Baringo, Kericho, Bomet, Uasin-Gishu, Elgeyo-Marakwet, Pokot Magharibi, na Narok, pia zikitarajiwa kushuhudia mvua.
Wakenya wameshauriwa kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuepuka kutembea au kuendesha gari katika barabara zilizojaa maji.
Jumapili wiki hii Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPS ilisema watu takriban 18 waliaga dunia kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Eneo la Mashariki ndilo lililoongoza kwa vifo hivyo ikiwa na jumla ya vifo 9 ikifuatwa na eneo la kati mwa nchi iliyonakili vifo vitatu, eneo la pwani viwili, Nairobi viwili na eneo la bonde la ufa viwili.









