Wahubiri Wadai Haki Kwa Mwenzao Aliyeuwawa Nakuru

0

Wahubiri wa madhehebu mbalimbali wamekashifu vikali mauaji ya Kasisi wa kanisa la PCEA Tabuga, eneo la Lanet, Julius Ndumia, wakieleza kuwa tukio hilo limeibua hofu kubwa miongoni mwa wakazi.

Kasisi Ndumia alipatikana ameuwawa na majambazi walioshambulia kanisa hilo na kuharibu mali ya kanisa.

“Kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu hali ya usalama katika eneo la Lanet na maeneo ya jirani, kumekuwa na ongezeko la kutia hofu la visa vya uhalifu, ikiwemo mauaji na ujambazi, hali ambayo imezua hofu na sintofahamu miongoni mwa wakazi.” Wahubiri wamesema.

Wametoa wito wa dharura kwa serikali na vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka na madhubuti.

“Tunatoa wito kwa serikali na asasi za usalama kuchukua hatua za haraka na ili kushughulikia hali inayozorota ya usalama katika eneo hili.”

Miongoni mwa mapendekezo yao ni pamoja na uchunguzi wa kina na wa haraka kuhusu mauaji ya kasisi huyo ili wahusika wawajibishwe, kuongezwa kwa uwepo wa maafisa wa usalama na wa kushika doria katika wadi ya Lanet Umoja na maeneo jirani, kuchukuliwa kwa hatua za mapema kudhibiti uhalifu unaoongezeka pamoja na kuimarishwa kwa taa za barabarani katika mitaa na barabara kuu.

Vilevile, wamewataka wananchi kudumisha utulivu na kushirikiana na vyombo vya usalama.

“Tunawaomba wananchi kudumisha utulivu na kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kuwabaini na kuwakamata wahusika.” Wahubiri wameongeza.

Haya yanajiri baada ya Kasisi huyo kuuawa tarehe 4 Mei na washukiwa wa ujambazi wanaodaiwa pia kuharibu mali ya kanisa hilo.

Wakazi, wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, wamekashifu tukio hilo wakilalamikia kuongezeka kwa utovu wa usalama katika eneo hilo.

“Nina huzuni kubwa sana kufuatia mauaji ya kasisi. Ikiwa kasisi anaweza kuuawa ndani ya makazi yake ya kanisa, basi ni lazima tutathmini upya hali ya usalama nchini.”

Aidha wametoa wito kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua dhidi ya wahalifu.

“Tunamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa DCI kutuma kikosi maalum kutoka Nairobi kuja hapa, kwa sababu hatuna imani na maafisa waliopo. Inawezekanaje watu wauwawe na hakuna anayekamatwa?”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here