Simanzi, familia ya raga nchini yaomboleza

0
Oloo (awali) katika mahojiano.

Kocha mkuu wa zamani wa Kenya Lionesses na mchezaji wa Nakuru RFC, Felix Oloo, amefariki dunia baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani nchini Marekani.

Shirikisho la Raga nchini limetangaza kifo chake likimtaja kama mtu aliyekuwa akiheshimika sana na aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mchezo huo nchini.

Oloo aligongwa na gari alipokuwa akijaribu kuvuka barabara ya Interstate 405 huko Bothell, Washington, katika tukio la Jumatatu tarehe 4 Mei asubuhi ambalo bado linafanyiwa uchunguzi.

Kwa mujibu wa klabu ya Nakuru Rugby FC, Oloo alifariki kufuatia ajali hiyo ya kusikitisha.

“Kwa masikitiko makubwa, familia ya Nakuru Rugby inatangaza kifo cha ghafla cha Felix Ade Oloo tarehe 4 Mei 2026 kufuatia ajali mbaya ya barabarani,” Nakuru RFC ilitangaza.

Oloo alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mchezo wa raga jijini Nakuru na pia aliwahi kuwa kocha wa Kenya Lionesses.

“Felix alikuwa mtumishi aliyejitolea wa mchezo huu, kocha, mshauri na kiongozi ambaye mchango wake kwa Nakuru Rugby na jamii pana ya raga ulikuwa mkubwa sana.

“Mapenzi yake kwa mchezo, kujitolea kwake kuendeleza wachezaji, na ari yake isiyotetereka iliwahamasisha wengi ndani na nje ya uwanja,” Nakuru RFC iliongeza.

Oloo aliichezea Nakuru RFC kati ya mwaka 2003 hadi 2017 na alikuwa sehemu ya vikosi vilivyoshinda Kenya Cup mwaka wa 2013 na 2014.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here