Kikosi cha mwisho cha maafisa wa polisi wa Kenya waliohudumu chini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) katika Misheni ya Pamoja ya Usalama nchini Haiti kimerejea nchini.
Ndege ya shirika la Kenya Airways ilitua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta Jumanne tarehe 28 Aprili jioni, ikiwa imewarejesha nyumbani maafisa wa kikosi cha mwisho waliobaki baada ya takribani miaka miwili ya huduma katika taifa hilo.
Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa Monica Juma alithibitisha kuondoka na kuwasili kwao, akiwapongeza maafisa hao kwa kujitolea na weledi wao katika utekelezaji wa jukumu hilo.
“Jana jioni (Jumatatu) saa kumi na mbili kwa saa za Haiti, kikosi cha mwisho cha Ken-Pol kiliondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toussaint Louverture kwa ndege maalum ya KQ kurejea nyumbani,” alieleza Juma.
“Maafisa hao, wakiwa katika eneo la operesheni kwa miezi 22, walihudumu kwa uaminifu na ujasiri katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba wameipa Kenya heshima kubwa katika jumuiya ya mataifa. La muhimu zaidi wamewasha mshumaa wa imani kwa taifa la Haiti sambamba na kuweka msingi wa hatua itakayofuata ya uthabitishwaji wake.” Aliongeza.
Juma pia alisifu uongozi wa kimkakati wa rais William Ruto katika kuunga mkono ushiriki wa Kenya katika operesheni hiyo ya kimataifa.
Maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja walikuwa Port-au-Prince mnamo Jumatatu kusimamia hatua ya mwisho ya kuondoka kwa kikosi hicho.
Kikosi cha pamoja cha usalama nchini Haiti kilichoongozwa na Kenya kililenga kurejesha utulivu na kupambana na magenge ya uhalifu ambapo katika kilele chake kilikuwa na zaidi ya maafisa 800 wa Kenya wakisaidiwa na wanajeshi kutoka nchi mbalimbali.
Baada ya kuondoka kwa kikosi hicho, jukumu la kudumisha usalama nchini Haiti litachukuliwa na kikosi kipya cha maafisa 5,500 kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambacho kinatarajiwa kuendeleza msingi uliowekwa na operesheni iliyoongozwa na Kenya.









