Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata ametimuliwa kutoka wadhifa wa kiranja wa wengi katika bunge la seneti na nafasi yake kutwaliwa na seneta wa Kiambu Kimani Wamatang’i.
Uamuzi wa kumfurusha Kang’ata umeafikiwa kwenye mkutano wa maseneta wa Jubilee ambao umeongozwa na katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju ambaye amemtuhumu Kang’ata kwa kutumia njia zisizofaa kuwasiliana na kiongozi wa chama Rais Uhuru Kenyatta.
Tuju amesema pia kuwa seneta huyo amekuwa akitoboa siri za chama hicho kwa wanahabari, hatua ambayo anasema inaenda kinyume na msimamo wa chama.
Hata hivyo Kangata amejitetea kuhusiana na madai hayo na badala yake kusema anafurushwa kufuatia barua yake kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyedai kuwa ripoti ya BBI si maarufu katika eneo la Mlima Kenya.