Naibu rais William Ruto ameendelea kujipigia debe kumrithi rais Uhuru Kenyatta akisema yuko tayari kupambana na yeyote wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2022.
Akizungumza alipopelekea kampeini za Hasla katika eneo la Port Victoria kaunti ya Busia, Ruto amesisitiza kuwa uongozi wake utawaleta pamoja Wakenya wote.
Ruto kwa mara nyingine amelaumu mchakato wa kufanyia katiba marekebisho kupitia BBI akisema umehujumu ajenda ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.
Yakijiri hayo
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alasiri hii anatazamiwa kuanza kampeini za kumpigia debe Agnes Kavindu anayewania wadhifa wa useneta katika kaunti ya Machakos.
Kalonzo anatazamiwa kujumuika na wenzake Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Gideon Moi wa chama cha KANU na Moses Wetangula wa chama cha FORD K.
Hii leo vigogo hao wa kisiasa wanatarajiwa kuhutubia mikutano ya hadhara katika maeneo ya Tala, Katangi, Kithimani na kisha kumalizia mjini Matuu.
Na huku wapiga kura wakitazamiwa kuelekea debeni Machi 18, kivumbi kinatarajiwa kuwa baina Mutua Katuku wa Maendelea Chap Chap, Kavindu wa Wiper na Urbanus Ngengele wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta Boniface Kabaka Disemba mwaka jana.