Naibu rais William Ruto amewaongoza viongozi wengine kumuombea afueni ya haraka kinara wa chama cha ODM Raila Odinga baada yake kupatwa na ugonjwa wa corona.
Akinukuu kitabu cha Isaya 53:5, Ruto amesema Raila wakati wowote ameonyesha ujasiri na kuibuka shujaa katika magumu yote aliyokumbana nayo.
Ruto ambaye amemtaja Raila kama rafikiye amemuombea afueni ya haraka akisema taifa nzima linamuombea.
Naye kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amemtakia Odinga uponyaji wa haraka akisema anazidi kumuombea.
Odinga katika taarifa amedhibitisha kuwa amekutwa na ugonjwa huo baada ya kupimwa zaidi ya mara moja na sasa yuko kwenye karantini kulingana na taratibu za wizara ya afya.
Waziri huyo mkuu wa zamani amepatwa na corona siku chache baada ya kuongoza misururu ya kupigia debe mswada wa marekebisho ya katiba BBI katika eneo la Pwani.









