Naibu rais William Ruto ametoa changamoto kwa idara ya mahakama kufanya kazi kwa uhuru kama ilivyo kikatiba pasipo kuingiliwa na asasi zingine za serikali.
Akizungumza katika mazishi ya mwanawe mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri Kinyanjui, Ruto amesema kuwa majaji na mahakimu wako na uwezo wa kufanya kazi bila kuingiliwa na mtu yeyote.
Ruto vilevile amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na vitengo vingine vya usalama kufanya kazi yao kwa kuhakikisha usalama kwa Wakenya wote bila kuegemea mirengo ya kisiasa.
Matamshi ya Ruto yanajiri siku moja baada ya waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i kuilaumu mahakama kwa kuchangia katika kuongezeka kwa uhalifu nchini kupitia kuwaachilia kwa dhamana wanapofikishwa mahakamani.