Usalama umeimarishwa nje ya majengo ya bunge la kaunti ya Migori huku mchakato wa kumuondoa gavana wa kaunti hiyo Zachary Okoth Obado ukianza.
Wawakilishi wadi wanarejea kutoka kwa likizo ya mwezi mmoja huku kiongozi wa wengi katika bunge hilo Ken Ouma akitazamiwa kuwasilisha notisi ya kulifahamisha bunge kuhusu hoja ya kumuondoa gavana huyo.
Ouma ambaye anazingatia uamuzi ulioafikiwa kufuatia mkutano wa chama cha ODM anasema mchakato huo utaendelea licha ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya wawakilishi wadi kutishiwa maisha.
Mchakato huo utampa nafasi spika wa bunge la kaunti hiyo kuratibu tarehe ya kujadiliwa kwa hoja hiyo ambapo gavana Obado aliyeshtakiwa kwa ufisadi atapewa nafasi ya kujitetea.
Haya yanajiri huku baraza kuu la vijana kutoka kaunti hiyo ya Migori likiongozwa na Julius Omamba likitaka mchakato wa kumbandua Obado kuharakishwa ili kuondoa hali ya sintofahamu inayowakumba wakaazi wa kaunti hiyo.