Waliokuwa vinara wa muungano wa upinzani NASA Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Raila Odinga wamekosania madeni ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Urafiki baina ya wanne hao umepasuka kufuatia matamshi ya Odinga kwamba hatamuunga mkono yeyote kwa sababu walimsaliti wakati wa uapisho wake pale Uhuru Park.
Akimjibu Odinga, Mudavadi kupitia msemaji wake Kibisu Kabatesi amemtaja Raila kama tapeli wa siasa na mtu asiyeaminika.
Huku akisisitiza kwamba hana haja ya kuungwa mkono na kuwa hakuna aliye na deni lake, Mudavadi anasema Raila hafai kuwasuta wenzake ambao walimsaidia kujiimarisha kisiasa.
Kiongozi huyo wa chama cha Amani National Congress (ANC) anasema anajuta kutumiwa vibaya na kuhadaiwa na Raila.
Matamshi ya Mudavadi yanaungwa mkono na mwenzake wa chama Wiper Kalonzo Musyoka ambaye anasema hataki kuungwa na yeyote katika azma yake ya kuwa rais.
Hata hivyo chama cha ODM kupitia katibu wake mkuu Edwin Sifuna kimtetea kiongozi wake na kuwataka Kalonzo, Mudavadi na Wetangula kutafuta kura kutoka kwa Wakenya kote nchini badala ya kumtumia Raila kama kisingizio.