Baraza la Magavana limetofautiana na taarifa ya waziri wa fedha Ukur Yattani kuwa serikali za kaunti zimepokea mgao wa shilingi billion 133 hadi kufikia sasa.
Katika taarifa, mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya amesema ni shilingi billion 93.9 pekee ambazo wamepokea na anaitaka hazina hiyo kuharakisha kutoa shilingi billion 89.6 zilizosalia.
Oparanya anasema pesa walizopokea hadi kufikia sasa ni matumizi ya hadi mwezi wa Oktoba kumaanisha kuwa kaunti zimekuwa bila pesa za matumizi kwa muda wa miezi tatu sasa.
Oparanya amesema pia kuwa hawawezi kutumia salio la shilingi billion 34.6 zilizoko katika benki kuu kwani anasema pesa hizo ni za kumalizia miradi ya maendeleo ambayo inaendelea.
Magavana wanasema shughuli katika serikali za kaunti huenda zikakwama iwapo serikali kuu haitatoa pesa zote.