Kenya inalenga kutoa chanjo dhidi ya virusi vya corona kwa watu wapatao milioni 1.25 katika awamu ya kwanza itakayoanza Februari hadi Juni mwaka huu.
Katibu mkuu katika wizara ya afya Dkt. Mercy Mwangangi anasema watakaokuwa wa kwanza kupewa chanjo hiyo ni wahudumu wa afya na wafanyakazi wa umma wanaofanya kazi katika vituo vya afya vya umma na vile vya kibinafsi.
Wafanyikazi katika idara ya usalama sawa na uhamiaji vile vile watapewa kipau mbele chanjo hiyo itakapoanza kutolewa.
Awamu ya pili inayotarajiwa kuanza kati ya Julai 2021 hadi Juni 2022 itawalenga watu milioni 9.7 walengwa wakiwa ni watu walio na umri wa miaka hamsini na zaidi na wale na umri wa miaka kumi na minane na zaidi ila wana matatizo mengine ya kiafya.
Watakaolengwa katika awamu ya tatu ni watu milioni 4.9 wanaoishi katika maeneo kuliko na watu wengi.
Wakati hayo yakijiri
Kenya imeripoti visa vipya 141 vya corona kati ya sampuli 5,644 zilizopimwa katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita na kufikisha idadi ya visa hivyo nchini kuwa 100,563.
Idadi ya waliopona imeongezeka na kufikia 83,821 baada ya kupona kwa watu 64 zaidi huku idadi ya maafa ikisalia kuwa 1,753 baada ya kutoripotiwa kwa maafa hii leo.